AZAM FC YARUDI KILELENI LIGI KUU BARA
KLABU ya Azam imerudi kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1, dhidi ya Coastal Union.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam, Coastal ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Semkufo Charles dakika ya 68 huku lile la Azam likifungwa na nyota wa kikosi hicho, Feisal Salum 'Fei Toto'.
Azam ambao ni mchezo wake wa 20 msimu huu, imeishusha Yanga hadi nafasi ya pili na pointi 43 ingawa imecheza michezo 16.
Bao la Feisal linamfanya kuendelea kuongoza kwenye mbio za ufungaji akifikisha mabao 12, nyuma ya Stephane Aziz KI wa Yanga mwenye 10 huku kwa upande wa Semkufo Charles akiendelea kufanya vizuri na kikosi hicho baada ya kufikisha mabao manne.
Kwa upande wa Coastal inaendelea kushikilia nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kufikisha jumla ya pointi zake 27 sawa na Tanzania Prisons iliyoifunga Simba mabao 2-1, mechi ya mapema ila zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mchezo wa Coastal Union ni wa 19 wa Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo kati ya hiyo imeshinda saba, sare sita na kupoteza pia sita.