Mastaa watatu wa Azam FC waliokwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu katika hospitali ya Vincent Pallott wamerejea nchini na wanaendelea vizuri na hivi karibuni watajumuika na wenzao uwanjani.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema kiungo Sospeter Bajana, beki Malickou Ndoye na mshambuliaji Franklin Navarro wamerejea nchi na wanaendelea vizuri kwani matibabu ya mastaa hao yalienda vyema, hawakufanyiwa upasuaji na sasa wanafanya mazoezi tiba (physiotherapy).

“Navarro, Malickou na Bajana wamerejea nchini, hata kwenye mechi dhidi ya Yanga walikwenda kutazama mchezo, kati yao waliorejea hakuna aliyefanyiwa upasuaji, wanaendelea vizuri, walishauriwa na daktari kupumzika na Machi 28 wataanza rasmi mazoezi ya uwanjani na wenzao”.

Mastaa hao walisafiri kwenda Afrika Kusini Februari 22 wakisumbuliwa na majeraha mbalimbali waliyoyapata.

Mcolombia Navarro alipata jeraha la kifundo cha mguu (enka) katika mchezo dhidi ya Simba uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Februari 9, 2024, baada ya kufanyiwa madhambi na beki Kennedy Juma.

Bajana alipata majeraha ya nyonga katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa Desemba 11, 2023 kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambao Azam FC ilishinda kwa mabao 2-1.

Wakati Malickou alipata majeraha katika mchezo wa raundi ya kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na Azam kupoteza kwa mabao 3-2.

Kuhusu Allassane Diao, yeye bado yupo Afrika Kusini akiendelea na matibabu ya goti (ACL) ambapo alifanyiwa upasuaji hivi karibuni na ikielezwa atakaa nje ya uwanja kwa miezi saba hadi tisa.

Azam Fc itashuka dimbani kucheza mchezo wake wa 22, Aprili 13, 2024 dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa. Hadi sasa ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 47, pointi tano nyuma ya Yanga inayoongoza ligi kwa pointi 52.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement