KIUNGO mkabaji wa Yanga, Khalid Aucho amesema jogoo aliyepewa na shabiki wa timu hiyo kutoka Mbeya, Peter Henry Chiwanga ana uwezo wa kumla peke yake.

Zawadi hiyo amepewa na shabiki wa Yanga, baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons wa ushindi wa mabao 2-1.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo ya kuku, Aucho amemshukuru shabiki huyo na kuahidi kuendeleza ubora wake kwa kuipambania timu kufikia malengo.

"Ni nadra sana kiungo kuonwa na kupewa zawadi, hili limenipa faraja kwani mara nyingi washambuliaji ndio wamekuwa wakipata fursa hizi za zawadi kutokana na kufunga;

"Nimefurahi kuipokea zawadi niliyopewa na kuhusu kumla na nani hii ni mipango yangu, lakini kwangu kula kuku mzima ni kawaida ni kutokana na namna ninavyofanya mazoezi," amesema.

Akizungumzia kiwango chake Aucho amesema "Nimeajiriwa kucheza na walinichukua kutokana na ubora niliokuwa nao, hivyo nitaendelea kupambana kuwa bora ili kuhakikisha nafanya kilicho bora."

Aucho alitoa pasi safi kwa Yao ambaye alimwaga maji kwa Pacome Zouzoua na kukwamisha mpira nyavuni akifunga bao la pili na la ushindi kwa Yanga.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement