Khalid Aucho ametibua hesabu za kocha Miguel Gamondi kwenye kikosi cha Yanga baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti utakaomfanya awe nje ya uwanja kwa wiki tatu.

Kwa muda ambao Aucho atakuwa nje ya uwanja atakosa mechi zisizopungua tatu, ikiwamo ya wapin-zani wao kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC, yenye staa matata kabisa kwa sasa, Feisal Salum 'Feitoto'.

Mechi nyingine atakazokosa, ukiweka kando ile ya Namungo ni pamoja na Ihefu na Geita Gold.

Aucho aliyeumia katika mechi ya mwisho ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, ambapo Yanga ilichapwa 1-0.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa timu yake imethibitisha kufanyiwa upasuaji huo.

"Tutamkosa Daktari wa Mpira (jina utani la Aucho) kwa wiki tatu kutokana na upasuaji aliofanyiwa hivyo mashabiki na wanachama wa timu yetu tunaomba mumuombee mchezaji wetu aweze kurudi kwenye majukumu yake mapema," imesomeka taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa klabu hiyo ya Yanga iliyongeza kuwa;

"Upasuaji umekwenda vizuri na mchezaji wetu yupo kwenye hali nzuri kinachotakiwa sasa ni kupata mapumziko kwa muda aliopewa ili aweze kurudi akiwa katika hali nzuri na ya ushindani."

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amethibitisha ni kweli mchezaji huyo amefanyiwa upasuaji baada ya kugundua tatizo hilo ambalo alilipata kwenye mchezo dhidi ya Al Ahly.

Amesema kwa mujibu wa taarifa za awali za daktari mchezaji huyo atakuwa nje kwa wiki tatu akiuguza jeraha hilo, huku akikosa mechi tatu zijazo za Ligi Kuu kabla ya kusimama kupisha kalenda ya FIFA na mechi za kimataifa za timu ya taifa. Mechi tatu zijazo za Yanga ni dhidi ya Ihefu FC iliyowafumua mabao 2-1 zilipokutana Highland Estate Mbarali jijini Mbeya, Geita Gold na Azam FC iliyopangwa kupigwa Machi 17.

Katika mechi za kwanza Geita ilifungwa mabao 3-0 na Yanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na iliipasua Azam mabao 3-2 Uwanja wa Azam Complex na timu hiyo kabla ya mechi ya leo jioni ilikuwa nafasi ya pili ikiwa na pointi 43 nyuma ya Azam yenye 44.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement