Beki wa zamani wa England, Ashley Cole amemtaka kocha wa Three Lions, Gareth Southgate kumpiga chini Bukayo Saka ili amwanzishe Phil Foden kwenye winga ya kulia katika mechi zao zijazo katika fainali za Euro 2024.

Saka, ambaye ni mchezaji bora wa mwaka wa England mara mbili, alianzishwa kwenye upande wa kulia katika mechi mbili ilizocheza England kwenye hatua ya makundi, huku Foden akianzia kushoto.

Hakuna mchezaji yeyote baina yao aliyefunga bao, licha ya kwamba Saka alitengeneza bao la Jude Bellingham kwenye mechi yao ya kwanza dhidi ya Serbia. Foden, alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu kwenye Ligi Kuu England baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa Manchester City.

Lakini, ameshindwa kuonyesha makali ya maana kwenye kikosi cha England huko kwenye Euro 2024 na sasa kocha Southgate ameombwa atafute namna. Kuna baadhi wanadhani mchezaji huyo amechezeshwe katikati, huku Bellingham arudi chini.

Lakini, Cole amekuwa na wazo la kumtoa kafara Saka, ili Foden aanze kwenye upande wa kulia.

"Ningependa kumwona Anthony Gordon akicheza kushoto, ningependa kumwona Foden akicheza kulia, kwa sababu ni maeneo watakayoonyesha viwango vyao bora," alisema Cole.

"Unaweza kufanya hivyo kwa kumpumzisha Saka. Ningependa kuona Foden akionyesha ulimwengu yeye ni bora kiasi gani kwa sasa. Sifurahishwi na kumkosoa mchezaji anayechezeshwa kwenye nafasi asiyomudu vyema. Watu wanaweza kusema ni mchezaji wa kiwango cha dunia, lakini unahitaji kuzoea pia. Kwa namna ninavyoona anavyocheza Man City, anapaswa kuchezeshwa kwenye eneo hilo.

"Kwenye sehemu ya kiungo au mabadiliko mengine, ningependa kumwona Kobbie (Mainoo) au Cole Palmer wakianza kwenye kiungo, lazima uwe na nguvu kwenye eneo hilo na kumiliki mpira, hayo ndiyo mabadiliko yangu ningefanya kwenye kikosi."

Kwa kuvuna pointi nne kwenye mechi mbili za makundi, England bado haijajihakikishia nafasi kwenye hatua ya 16 bora endapo kama itapoteza mchezo wa mwisho wa hatua hiyo ya makundi dhidi ya Slovenia. Gary Neville amekuwa tofauti na Cole baada ya kudai kwamba Foden ndiye anayepaswa kuanzishiwa benchini kwenye mchezo huo wa mwisho wa makundi utakaofanyika usiku wa leo Jumanne.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement