Nyota wa kimataifa wa Ivory Coast aliyesajiliwa dirusha dogo la usajili, Joseph Guede ameifungia Yanga mabao mawili ikiichapa Polisi Tanzania mabao 5-0, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo wa Kombe la Azam Sport Federation Cup (ASFC), umeshuhudia Yanga ikiendeleza moto wake wa kuzichapa timu zinazokutana nazo mabao matano, ukiwa ni ushindi wa pili wa idadi hiyo ya mabao kwenye michuano hii baada ya awali kuifunga Hausung mabao 5-1 kwenye mchezo wa hatua ya pili.

Guede amefunga mara mbili mabao yake ya kwanza ndani ya timu hiyo kwenye dakika za 13 na 45+1 yote akiyafunga kwa kichwa akitumia krosi za winga Augustine Okrah.

Winga Farid Mussa aliipa Yanga bao la pili dakika ya 32 akitumia krosi ya kiungo mshambuliaji Stephanie Aziz KI na kuifanya timu yao kwenda mapumziko ikiwa na uongozi wa mabao hayo 3-0.

Kipindi cha pili Yanga ilipata bao la nne kupitia mshambuliaji wake Clement Mzinze akimalizia krosi ya beki wake wa kulia Kibwana Shomari dakika ya 82 kabla ya kiungo mshambuliaji, Shekhan Khamis kumalizia msumari wa tano kwa penalti baada ya Mzinze kuangushwa akiwa anaenda kufunga.

Bao hilo la Mzinze limemfanya kufikisha manne msimu huu baada ya awali kupiga mabao matatu Hat trick kwenye mchezo wa hatua ya pili.


You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement