ANTONIO CONTE ANATARAJIWA KUTANGAZWA KUWA KOCHA WA NAPOLI
Antonio Conte anayetarajiwa kutangazwa kuwa kocha mpya wa Napoli siku chache zijazo, amependekeza jina la straika wa Chelsea na timu ya taifa ya Ubelgiji, Romelu Lukaku ili asajiliwe katika dirisha hili la majira ya kiangazi ili kuboresha eneo lao la ushambuliaji.
Conte anamfahamu vizuri Lukaku kwa sababu aliwahi kuchukua naye ubingwa mwaka 2021 akiwa na Inter Milan na staa huyu alionyesha kiwango bora sana.
Lukaku ambaye msimu huu amecheza mechi 47 za michuano yote na kufunga mabao 21, mwaka huo 2020/21 alicheza mechi 44, akafunga mabao 30 na kutoa asisti 10.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026, lakini Chelsea ipo tayari kumuuza ikiwa itapata ofa sahihi kwani benchi la ufundi halijaonyesha kumwitaji aendelee kuwepo.
Lukaku pia ametajwa kuwa katika orodha ya mastaa ambao matajiri wa Saudi Arabia wanataka kuwasajili katika dirisha hili.
Lukaku amekuwa mmoja wa washambuliaji bora duniani miaka ya karibuni na ameshapita kwenye timu nyingine kubwa ikiwamo Manchester United na Kocha Conte anaamini uwepo wa nyota huyo msimu ujao Napoli utaisaidia kurejesha taji lao walilolipoteza mwisho wa msimu uliomalizika.