Serikali imetoa Sh286 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu mkoani Arusha uliopewa jina la Dk Samia Suluhu Hassan utakaojengwa na Kampuni ya China Railway Construction Engineering Group Limited (CRCEG) kutoka nchini China.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amesema hayo leo Machi 19, 2024 wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa uwanja huo.

Dk Ndumbaro amesema kuwa uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuingiza watu 30,000 na ni wa kisasa zaidi katika nchi za Afrika Mashariki.

Amesema Serikali itahakikisha ujenzi huo unafanywa kwa haraka kwa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon), ifikapo mwaka 2027, ikiwa ni juhudi za Rais Samia.

"Uwanja huo utakuwa na ubora wa hali ya juu kwani utakuwa na vyumba vya watu mashuhuri pande zote mbili za uwanja zoezi hili limefanyika leo ambapo, Rais Samia akiwa anatimiza miaka mitatu ya uongozi wake,” amesema Dk Ndumbaro.

Ameipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kwa juhudi ilizofanya mpaka kukamilisha kuanza kwa ujenzi huo ambao umechukua muda mrefu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko amewataka wakandarasi wa uwanja huo wahakikishe ujenzi unakamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement